Wednesday, February 26, 2020

Hadithi ya Kitenge

Image result for fashion za kitenge

Kitenge ni aina ya kitambaa kilichotengenezwa kwa material ya pamba ambacho kina michoro na urembo wa maumbo na rangi mbalimbali. Neno "Kitenge" ni neno la Kiswahili, na hutumika zaidi katika nchi za Afrika Mashariki. "Chitenge" ni neno linalotumka kama m'badala wa Kitenge kwenye nchi za Malawi na Zambia.



Katika nchi za Ulaya na Marekani, Kitenge kimefananishwa na "Khanga" ... yaani, wameshindwa kutofautisha baina ya aina hizi mbili za nguo. Muangaliaji wa kawaida, anaweza kufikiri kuwa kweli Kitenge na Khanga ni kitu kimoja. Hii inaweza kuwa inatokana na aina ya urembo/michoro iliyopo kwenye nguo hizi. Tofauti moja na ya kwanza ya kutenganisha nguo hizi ni; Khanga huwa zina "maandishi" au "semi" za Kiswahili. Kitenge hazina maneno haya. Tofauti nyingine kubwa kati ya Kitenge na Khanga ni kuwa kitambaa cha Khanga ni chepesi zaidi unapokigusa.

Kiutamaduni, mavazi ya Kitenge yametumika zaidi Afrika Mashariki na Kati. Nchi kama Nigeria, Ghana, Togo, Congo, Rwanda, Burundi, Tanzania, Uganda na Kenya ni kati ya nchi chache Afrika ambapo utakuta wakivaa vazi la Kitenge. Kutokana na utandawazi, hivi sasa si ajabu kuona mavazi yaliyotengenezwa kwa Kitenge yakiwa yamevaliwa na watu kutoka nje ya Afrika.

Vazi la Kitenge limepata umaarufu kiasi kwamba hivi sasa katika ulimwengu wa mitindo ya mavazi linashindana na mavazi ambayo kihistoria yalikuwa yameshika umaarufu zaidi. Wanamitindo wa ndani na nje ya Afrika wanatumia mbinu na ujuzi wa hali ya juu kutengeneza nguo za kike na hata nguo za kiume kwa kutumia material hii. Vitambaa vya magauni vya kila siku imekuwa sio dili tena.

Uzuri wa vazi hili ni kwamba linaweza likavaliwa na mtu yeyote, sehemu yeyote. Vazi la kitenge linaweza kutengenezwa kama nguo za watoto wa kike au nguo za watoto wa kiume. Linaweza likavaliwa ofisini, kanisani au kama nguo ya kushindia. Vazi la kitenge limetokea kupendwa sana kutokana na "prints" zake zenye mahadhi ya Kiswahili na maumbo ya asili yenye rangi maridhawa za kuvutia. Angalia video hii upate kujionea jinsi akina dada wanavyopendeza ndani ya mashono mbalimbali ya vazi la Kitenge.

No comments:

Post a Comment