Vipodozi vya asili vimekuwepo toka enzi na enzi. Katika miaka ya 80, wakina mama walitumia sana magamba na majani ya miti yaliyosagwa kama aina fulani fulani ya vipodozi. Leo hii, bado tunaona baadhi ya makabila ya Tanzania yakitumia michanganyiko mbalimbali kwa mfano, mafuta ya samli, maparachichi nk kama vipodozi vya kulainisha ngozi.
Uwepo wa uhitaji (demand) wa vipodozi vya asili umechochewa sana kuwepo kwa aina nyingi za vipodozi vya viwandani ambavyo havikidhi viwango. Tumeshuhudia matangazo na kampeni kadha wa kadha za vipodozi ambavyo baadae vimekuja kugundulika kuwa na sumu zinazomsababishia mtumiaji kupata saratani ya ngozi au hata uzazi.
Vipodozi vya asili vina faida kadhaa tofauti na vipodozi ambavyo si asilia. Kwa mfano, faida moja kubwa ni kutokuwepo kwa sumu zinazosababisha magonjwa. Faida ya pili ni unafuu wa bei na faida kubwa ya tatu ni urahisi wa kupatikana. Hata hivyo, ikumbukwe kuwa kuna baadhi ya makampuni au watu binafsi ambao wameanza kutengeneza na kufungasha vipodozi kisha wakaviita "vya asili". Tunapozungumzia vipodozi asili hapa tunamaanisha vipodozi ambavyo havijachanganywa na kemikali yoyote ya kiwandani.
Baadhi ya mazao au mimea ambayo imekuwa mashuhuri katika kutengeneza vipodozi asili ni pamoja na:
- Tumeric
- Vitunguu maji
- Parachichi
- Mdalasini
- Mpapai
- Tangawizi
- Limao
- Matango
- Asali
Inawezekana muonekano au harufu yake ikawa sio sawa na ile ya vipodozi vya viwandani, lakini matokeo ya utumiaji yakawa mazuri zaidi. Tutawaletea makala ya jinsi ya kuchanganya mimea ili upate kipodozi cha asili kisicho na madhara kwenye mwili wako.
No comments:
Post a Comment